Nifanye Nini Ninapohisi Sijafikia Hatua Niliyotarajia Maishani?

Watu wengi huishi na hisia za kwamba maisha yao hayasongi mbele kama walivyotarajia.

Huenda unaona marafiki zako wanafunga ndoa, wanapiga hatua katika kazi zao, wananunua nyumba, au wanafikia mambo ambayo ulitarajia na wewe ungekuwa umeyafikia kufikia sasa.

Katika ulimwengu uliojaa kulinganisha maisha na shinikizo la kufikia mafanikio, ni rahisi kuvunjika moyo au kuhisi kutokuwa na uhakika unapowaona wengine wakisonga mbele huku wewe ukihisi kama umesimama sehemu ile ile.

Lakini ukweli ni huu—maisha yako sio mashindano.

Kila mmoja wetu ana safari yake ya kipekee. Maisha yetu hayapimwi kwa kulinganisha mafanikio yetu na ya wengine. Mungu hutimiza kusudi lake katika maisha yetu kwa wakati wake. Na wakati mwingine, kile kinachoonekana kama kuchelewa huwa ni maandalizi ya jambo kubwa zaidi.

Hata maisha yanapoonekana kutokuwa na uhakika, unaweza kuwa na amani ukijua kwamba Mungu hajakusahaulisha, wala hajalisahau kusudi alilonalo kwa maisha yako ya baadaye.

Basi ufanye nini unapohisi maisha yako hayasongi mbele kama ulivyotarajia? Hebu tuone jinsi Biblia inavyoweza kukusaidia kupata amani, kusudi, na mwelekeo katika kipindi hicho.

Tutajifunza:

Kwa nini kujilinganisha na wengine kunaweza kuharibu amani na kujiamini kwako

Watu wengi huhisi kama wamechelewa katika maisha kwa sababu wanalinganisha safari yao na maendeleo ya watu wengine.

Unapozungumza na marafiki au unapotazama mitandao ya kijamii, unaweza kujikuta ukikumbana mara kwa mara na habari za mafanikio ya wengine. Inaweza kuonekana kana kwamba kila mtu anafikia mafanikio kwa haraka kuliko wewe. Lakini tatizo la kujilinganisha ni kwamba mara nyingi huangalia kile kinachoonekana kwa nje badala ya hali halisi iliyopo ndani.

Mara nyingi mitandao ya kijamii huonyesha mafanikio, hatua muhimu, na nyakati za furaha za watu, huku ikificha changamoto, kukatishwa tamaa, na vipindi vya kusubiri wanavyopitia. Hivyo, huenda unalinganisha maisha yako halisi na sehemu nzuri tu za maisha ya mtu mwingine zilizochaguliwa kuonyeshwa.

Haijalishi hali yako ikoje, ni muhimu kukumbuka kwamba kila mtu ana safari yake ya kipekee katika maisha. Wengine hufikia malengo yao ya kazi mapema, huku wengine wakigundua kusudi lao baadaye maishani. Wengine hufunga ndoa wakiwa vijana, wakati wengine hupitia kwanza kipindi cha kuwa peke yao na kujijenga. Safari moja haiwezi kupimwa kwa kulinganisha na safari nyingine.

Kujaribu kufanya hivyo kunaweza kutuondolea amani na kutukengeusha kutoka kwenye kusudi ambalo Mungu analo kwa maisha yetu.

Biblia inatupa onyo hili:

“Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake” (Wagalatia 6:4, SUV).

Furaha yako haipaswi kutegemea maendeleo unayoyaona kwa watu wengine. Amani ya kweli hupatikana unapojua thamani na utambulisho wako ndani ya Mungu, sio kwa kujaribu kufikia viwango au matarajio ya jamii.

Ikiwa kila mara unahisi kama hujafikia hatua unayotakiwa kuwa nayo, jiulize: Ninapima maisha yangu kwa vigezo vya nani?

Wakati mwingine shinikizo tunalohisi halitokani na Mungu, bali hutokana zaidi na matarajio ya jamii, familia, au ushawishi wa mitandao ya kijamii.

Na hilo linatupeleka kwenye ukweli mwingine muhimu ambao watu wengi huupuuza.

Biblia inasema nini kuhusu wakati wa Mungu

Teenagers studying the Bible outside their tent during a campout.

Biblia inatufundisha kwamba wakati wa Mungu hauongozwi na ratiba za wanadamu. Ingawa mara nyingi watu hupima maisha kwa umri, hatua walizofikia, au mafanikio yao, Mungu huangalia zaidi ukuaji wetu, tabia zetu, na kusudi lake katika maisha yetu.

Mhubiri 3:1 inasema:

“Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu” (SUV).

Aya hii inatukumbusha kwamba maisha yana vipindi tofauti. Kuna vipindi vya kusubiri, kujifunza, kupona, na kujiandaa. Pia kuna vipindi vya kukua, kupata fursa, na kuona matokeo ya juhudi zetu. Jambo fulani kutotokea bado haimaanishi kwamba halitatokea kamwe.

Watu wengi katika Biblia walipitia vipindi vya kusubiri kabla ya kuona utimilifu wa kusudi la Mungu katika maisha yao:

  • Yusufu alipitia miaka ya utumwa na kifungo gerezani kabla Mungu hajamwinua kuwa kiongozi mkuu nchini Misri.
  • Musa alikaa jangwani kwa miaka mingi kabla ya kuitwa kuwaongoza Waisraeli.
  • Daudi alipakwa mafuta kuwa mfalme muda mrefu kabla hajaanza kutawala.
  • Ibrahimu alisubiri kwa miaka mingi kabla ya kuona utimilifu wa ahadi ya Mungu ya kumpa mwana.

Kwa mtazamo wa kibinadamu, huenda maendeleo yao yalionekana kuwa ya polepole. Lakini Mungu alikuwa akitenda kazi kwa siri katika kila hatua ya safari yao.

Wakati mwingine kujihisi kama umeachwa nyuma katika maisha kunaweza kukuletea hofu kubwa kuhusu siku zako za baadaye au kukufanya upitie kipindi cha mashaka na wasiwasi. Unaweza kujiuliza ikiwa umepoteza muda au umekosa fursa muhimu. Lakini mipango ya Mungu haizuiliwi na ratiba yako au hatua ulizofikia katika maisha.

Isaya 60:22 inasema:

“Mdogo atakuwa elfu, Na mnyonge atakuwa taifa hodari; Mimi, BWANA, nitayahimiza hayo wakati wake” (SUV).

Haimaanishi kwamba tunapaswa kuacha kujitahidi kufikia malengo yetu. Inamaanisha tunajifunza kutafuta maendeleo bila hofu au msukumo wa kujilazimisha kupita kiasi. Kumtumaini Mungu na wakati wake hutusaidia kubadilisha shinikizo kuwa amani.

Lakini tunawezaje kutumia jambo hili katika maisha yetu ya kila siku?

Jinsi ya kuacha kupima maisha yako kwa kulinganisha na ya wengine

Kuondokana na kujilinganisha na wengine kunahitaji kubadilisha namna unavyofikiri. Badala ya kuangalia hatua ambazo wengine wamefikia, zingatia safari yako mwenyewe na mtu ambaye Mungu anakujenga kuwa.

Njia moja halisi ya kupunguza kujilinganisha na wengine ni kupunguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii. Hii haimaanishi kwamba mitandao ya kijamii ni mibaya. Lakini kuendelea kutazama maudhui yanayokufanya ujione hufai au hujafikia kiwango fulani kunaweza kuathiri hali yako ya kihisia na kukufanya uwe na mtazamo usio sahihi kuhusu mafanikio.

Huenda unajiuliza, “Itakuwaje kama kuna watu aambao wamepiga hatua mbele yangu?”

Hata kama wengine wanaonekana kupiga hatua kwa haraka zaidi kuliko wewe, thamani yako haijapungua. Mafanikio hayapimwi tu kwa fedha, ndoa, mafanikio ya kikazi, au kutambuliwa na watu. Maisha yenye maana hujengwa juu ya uaminifu, tabia njema, amani, na kuishi kwa kusudi.

Warumi 12:2 inawahimiza waamini kutofuata mifumo na mwenendo wa dunia hii. Mara nyingi jamii huweka matarajio yasiyo halisi kuhusu ni hatua gani unapaswa kuwa umefikia katika umri fulani. Hata hivyo, wito wa Mungu kwa maisha yako unaweza kuwa tofauti na wa mtu mwingine.

Zifuatazo ni baadhi ya njia zinazoweza kukusaidia kuepuka kujilinganisha na wengine:

  • Jizoeze kuwa na moyo wa shukrani kwa baraka ulizonazo sasa na kwa maendeleo ambayo tayari umefanya.
  • Furahia mafanikio ya wengine bila kudharau thamani yako mwenyewe.
  • Elekeza umakini wako katika ukuaji binafsi badala ya kushindana na wengine.
  • Jitendee kwa huruma na ufahamu wakati unapopitia nyakati ngumu.
  • Kumbuka kwamba changamoto na vikwazo vya sasa haviamui mustakabali wako.

Kuwa na huruma kwa nafsi yako ni muhimu sana unapopitia kipindi cha kukata tamaa. Watu wengi hujizungumza kwa ukali wanapohisi kwamba wamechelewa au hawajasonga mbele kama walivyotarajia. Lakini ukuaji unahitaji uvumilivu. Kama ungemtia moyo rafiki anayepitia kipindi kigumu, jifunze pia kujipa moyo na kujitendea kwa wema huo huo.

Unapoacha kujishughulisha kupita kiasi na maendeleo ya wengine, utaweza hatimaye kuelekeza nguvu zako kwenye safari yako mwenyewe.

Njia za vitendo za kusonga mbele kwa kusudi na tumaini

Kujihisi kama umeachwa nyuma huwa mzigo mkubwa zaidi unapohisi kwamba umekwama. Hali hii inaweza kusababisha wasiwasi na kukata tamaa, na hatimaye kukufanya usiridhike na safari yako mwenyewe.

Wakati mwingine unapohisi hivyo, jambo bora unaloweza kufanya ni kuanza kusonga mbele kwa hatua ndogo lakini zenye kusudi.

Maendeleo sio lazima yaonekane kupitia matukio makubwa au mafanikio ya ghafla. Mara nyingi hujengwa polepole, kupitia uaminifu wetu katika mambo madogo ya kila siku, maamuzi sahihi tunayofanya, na hatua tunazochukua katika kukua kama mtu.

Wafilipi 3:13–14 inasema:

“Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie medali…” (SUV).

Mtume Paulo alijua kwamba ili mtu aendelee kukua, ni lazima asikwame katika majuto ya yaliyopita au hofu kuhusu siku zijazo.

Zifuatazo ni baadhi ya njia za vitendo zinazoweza kukusaidia kurejesha hamasa na kuendelea kusonga mbele unapohisi kwamba umeachwa nyuma katika maisha:

  1. Pitia upya maana yako ya mafanikio

Jiulize ikiwa malengo yako yanaakisi maadili na kusudi lako halisi, au kama yanachochewa zaidi na matarajio ya jamii. Kumbuka kwamba mafanikio yasiyoambatana na amani na kusudi mara nyingi huwaacha watu wakiwa na hisia za utupu.

Kumbuka kwamba Mungu anajali zaidi kuhusu mabadiliko ya tabia na utu wako kuliko namna unavyoonekana machoni pa watu.

  1. Weka malengo madogo na yanayowezekana kufikiwa

Ndoto kubwa zinaweza kuonekana kuwa nzito na kukatisha tamaa, hasa unapokuwa tayari unapitia hali ya kuvunjika moyo. Badala ya kuangazia tu hatua kubwa za mafanikio, zingatia hatua ndogo za maendeleo unazoweza kuchukua kila siku.

Kwa mfano:

  • Kuboresha eneo moja la taaluma yako.
  • Kuimarisha uhusiano wako na Mungu.
  • Kujenga tabia zenye afya zaidi.
  • Kujifunza ujuzi mpya.
  • Kuboresha afya yako ya kihisia na kiakili.

Kumbuka, hata maendeleo madogo bado ni maendeleo.

  1. Jizungushe na watu wanaokutia moyo

Watu unaochagua kuwa nao wana mchango mkubwa katika mtazamo wako na namna unavyoyaona maisha. Tumia muda pamoja na watu wanaokuchochea kukua, kupata hekima, na kudumisha tumaini, badala ya wale wanao kufanya ujilinganishe kila mara na wengine au kukuzunguka kwa mtazamo hasi.

Jamii yenye kujenga inaweza kukukumbusha kwamba safari yako bado ina thamani, hata wakati maisha yanaonekana kuwa na changamoto au kutokuwa na uhakika.

  1. Zingatia ukuaji wa ndani

Wakati mwingine tunaweza kujikita sana katika mafanikio ya nje kiasi cha kupuuza mabadiliko ya ndani ya maisha yetu. Hata hivyo, sifa kama vile uvumilivu, unyenyekevu, hekima, ustahimilivu, na imani zina thamani kubwa machoni pa Mungu.

Wakati unapitia nyakati ngumu, usiruhusu changamoto zikuvunje moyo. Kumbuka kwamba Mungu anaweza kutumia vipindi hivyo vigumu kukujenga, kukuimarisha, na kukuandaa kwa hatua inayofuata katika maisha yako.

Jinsi imani inavyoweza kusaidia wakati maisha yanapokuwa hayana uhakika

Silhouette of a man standing on top of a rock looking at the western horizon at sunset.

Photo by Diego Gennaro on Unsplash

Imani haiondoi changamoto au maswali kuhusu kesho, lakini hutupa nguvu ya kusonga mbele tukiwa na tumaini kwamba Mungu bado anaongoza safari yetu.

Unapohisi kwamba umeachwa nyuma, ni rahisi kuamini kwamba Mungu ameshindwa kutimiza mpango wake katika maisha yako. Lakini ukweli ni kwamba, kuchelewa, kukatishwa tamaa, na njia zisizotarajiwa havimaanishi mwisho wa safari yako wala kushindwa.

Yeremia 29:11 inasema:

“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (SUV).

Mungu anaona picha kamili ya maisha yako, wakati wewe unaweza kuona tu hali ya sasa unayopitia. Kumtumaini Yeye kunamaanisha kuamini kwamba safari yako bado ina kusudi, hata kama muda na hatua unazopitia ni tofauti na za marafiki zako au matarajio ya jamii.

Imani inakusaidia kuachilia shinikizo la kujaribu “kuwahi kufikia wengine” na badala yake kutembea katika mwendo ambao Mungu amekuandalia.

Aina hii ya amani hubadilisha namna unavyofikiri. Badala ya kuishi katika hofu ya kila mara kwamba umeachwa nyuma, unaanza kuthamini ukuaji unaoendelea ndani yako. Badala ya kukimbizana na hatua ambazo wengine wamefikia, unaanza kufuatilia wito ambao Mungu ameweka kwa ajili ya maisha yako mwenyewe.

Utagundua kwamba furaha haiji kwa kufikia malengo yako kulingana na muda uliouweka. Badala yake, furaha ya kweli inatokana na kutembea kwa ukaribu na Mungu katika kila kipindi cha maisha.

Safari yako bado haijafika mwisho

Kuhisi kwamba umeachwa nyuma katika maisha kunaweza kusababisha wasiwasi, kukata tamaa, na shinikizo, hasa katika utamaduni unaochochewa na kujilinganisha na wengine na mitandao ya kijamii.

Lakini thamani yako haitegemei kasi unayofikia hatua muhimu za maisha, wala namna safari yako inavyolinganishwa na safari za wengine.

Mungu ana njia ya pekee ya maisha kwa kila mtu. Ingawa wengine wanaweza kusonga kwa mwendo tofauti, hadithi yako bado inaendelea kuandikwa. Kuchelewa, changamoto, na kutokuwa na uhakika unazopitia leo vinaweza kuwa vinakuandaa kwa ukuaji wa ndani zaidi, imani iliyo imara zaidi, na kusudi kubwa zaidi.

Badala ya kupima maendeleo yako kwa kuzingatia matarajio ya jamii, kwa nini usilenge kuwa mtu ambaye Mungu anakuita uwe? Chagua kujitendea kwa huruma badala ya kujihukumu. Fwatilia malengo yenye maana ukiwa na amani badala ya hofu. Na uamini kwamba wakati wa Mungu una hekima zaidi kuliko matarajio ya wanadamu.

Haijalishi uko wapi katika safari yako, fahamu kwamba haujasahaulika, haujaondolewa katika mpango wa Mungu, wala hujachelewa kufikia mambo makubwa.

Ikiwa unatafuta faraja zaidi inayotokana na Biblia kuhusu kusudi na kutokuwa na uhakika wa maisha, tembelea sehemu ya Wakati Ujao katika Tumaini kwa Afrika. Huko utapata mwongozo wa vitendo unaoongozwa na imani, utakaokusaidia kukabiliana na changamoto za maisha kwa tumaini, hekima, na ujasiri.

Hapa kuna baadhi ya makala za kuanza nazo:

Haijalishi unapitia kipindi gani katika maisha, huhitaji kukabiliana nacho peke yako. Endelea kujifunza, endelea kukua, na endelea kumtumaini Mungu kwamba anaongoza safari yako kuelekea mbele.

Pin It on Pinterest

Share This